Sunday, December 2, 2012


 
  JE, KUSIFU NA KUABUDU NI KARAMA?

“Kila mwenye pumzi amsifu Bwana, Haleluya.” Zaburi 150:6

Kama kusifu na kuabudu ni karama basi kila mtu amepewa, lakini neno la Mungu linasema

“…basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbal…i”Warumi 12:6

Ukisoma tafsiri ya kiingereza ya Revised Standard Version inasema , ‘kwa kuwa tuna karama zilizotofautiana…..’ hii ina maana kila mtu anakarama yake ingawa wengine waweza kuwa na karama zaidi ya moja, kwa mantiki hiyo basi kusifu na kuabudu si karama na kama unaiita karama hii ni kukwepa kuwajibika juu ya wajibu wa kusifu na kumwabudu aliokupa yeye mwenyewe.  Mara nyingi nimekuwa nikisikia katika makanisa mbalimbali watu wakiwasifu waimbaji kuwa wanakarama ya kusifu na kuabudu, hii siyo kweli na ni HAPANA kubwa. Tukirejea katika mstari wa Biblia wa muongozo wetu wa kipengele hiki chenye swali ambalo linasema, Je kusifu na kuabudu ni karama?  Biblia inasema ‘kila mwenye pumzi na amsifu Bwana’ na si kila mwenye sauti nzuri.  Ukasoma tafsiri ya kiingereza inasema ‘kila chenye pumzi|’ na kama ingekuwa kila mwenye sauti nzuri sisi wenye sauti ya kukwaruza tusingeweza kumsifu na kumwabudu Bwana.  Kwa hiyo ufike mahali utambue kama mtoto na mtumishi wa Mungu, pumzi ambayo Mungu amekupatia ni kwa ajili ya kumsifu yeye tu, ila yule anayesimama mbele ya umati wa watu akiimba na kuongoza kusifu na kuabudu yeye amepewa karama ya kuongoza na si karama ya kusifu na kuabudu. Tufike mahali tutambue ya kuwa wote tunawajibu wa kusogea mbele za Mungu kumsifu na kumwabudu yeye kwasababu pazia la hekalu limekwisha pasuka.  Matt Redman kiongozi wa kusifu na kuabudu mmarekani anasema;

We had forgotten that we are all performers

of worship and that God is the audience”

Tafsiri yake kwa lugha ya Kiswahili ni hii ‘tumesahau kuwa sisi sote ni waabuduo na Mungu ndiye hadhira(mtazamaji)’.

Matt Redman alizungumza hivyo kwasababu aliliona tatizo ndani ya kanisa na katika makongamano mbalimbali ya uimbaji kuwa wamesahau kuwa Mungu ndiye hadhira, katika yote wanayoyafanya unapaswa kama mtumishi utambue ya kwamba Mungu unayemtumikia au unayemwabudu na kumsifu ni Mungu mwenye wivu na hawezi kuvumilia kama utakuwa unachukua hata sehemu ndogo ya utukufu wake.  Katika maandiko mengi tulioyapitia tunaona kuwa kumsifu na kumwabudu Mungu si karama kama wengine wangeweza kufikiri, bali kila mmoja anawajibika kumsifu na kumwabudu Mungu hasa tukirudi katika neno letu la muongozo katika kitabu hiki

”nao wamwabuduo yeye imewapasa…” Yohana 4:24b,

maana yake ni wajibu wa kila mmoja na si karama. Kwahiyo waweza kuwa Mungu amekukirimia kuimba au kuongoza lakini si kusifu na kuabudu. hiyo ni njia ya kukwepa wajibu na jukumu Mungu aliokupa hapa duniani. Tambua nafasi yako katika utumishi wako.

No comments:

Post a Comment